Russia inapanga kulipua bwawa kubwa la maji Ukraine, wanajeshi wa Iran wanasaidia kutekeleza mashambulizi

Picha ya Satellite inayoonyesha bwawa la kuzalisha umeme la Kakhovka, Nova Kakhovka. Febrauri 26, 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ametoa wito kwa mataifa ya Magharibi kuionya Russia dhidi ya mpango wake wa kulipua bwawa kubwa la maji, akisema kwamba hatua hiyo itasababisha mafuriko makubwa kusini mwa Ukraine.

Wanajeshi wa Ukraine wanajiandaa kupambana na wanajeshi wa Russia kwa lengo la kuwasukuma kutoka mji wa Kherson, katika hatua inayotajwa kuwa mhimu sana katika vita hivyo.

Zelenskyy amesema kwamba wanajeshi wa Russia wameweka mabomu ndani ya bwawa la Nova Kakhovka, linaloshikilia kiasi kikubwa cha maji na kwamba wanajeshi wa Russia wanapanga kulipua bwawa hilo.

"Kila mtu kote duniani ni lazima achukue hatua za nguvu na kwa haraka kuzuia shambulio la kigaidi la Russia. Kuharibiwa kwa bwawa hilo kutasababisha janga kubwa la kibinadamu,” amesema Zelenskyy.

Russia imedai kwamba Kyiv inapanga kulipua bwawa hilo.

Kamanda wa wanajeshi wa Russia nchini Ukraine Sergei Surovikin, amedai kwamba wanajeshi wa Ukraine tayari wametumia makombora ya Marekani dhidi ya bwawa hilo.

Ukraine imedai kwamba Russia inapanga kulipua bwawa hilo na kuilaumu Kyiv.

Hakuna upande umetoa ushahidi wa madai yake.

Kulipuliwa kwa bwawa hilo kutasababisha mafuriko makubwa katika makazi ya watu wanaoishi chini yake hasa katika mji wa Kherson, ambapo wanajeshi wa Ukraine wana matumaini ya kudhibithi kutoka kwa wanajeshi wa Russia.

Uharibifu wa bwawa hilo vile vile utasababisha uharibifu mkubwa kwenye mfumo wa usambazaji maji kuelekea kusini mwa Ukraine, ikiwemo Crimea ambayo Moscow iliinyakua kimabavu mwaka 2014.

Zelenskyy ametoa wito kwa viongozi kote duniani kueleza kwamba uharibifu wa bwawa hilo unastahili kuchukuliwa “sawa na matumizi ya silaha za uharibifu mkubwa,” jinsi ilivyo na athari za Russia kutumia silaha za nyuklia au kemikali.

Mikakati ya kukomboa Kherso

Ukraine imeweka marufuku ya kutoa habari kutoka Kherson, lakini kamanda wa wanajeshi wa Russia Surovikin, alisema wiki hii kwamba hali tayari ni ngumu sana na kwamba Russia inaweza kufanya maamuzi magumu sana.

Utawala wa Kremlin haujasema lolote iwapo rais Vladimir Putin alikuwa ametoa amri kwa wanajeshi wa Russia kuondoka Kherson.

Jeshi la Russia limesema kwamba wanajeshi 2,000 waliosajiliwa hivi karibuni wamewasili Kherson kwa mapigano.

Viongozi wa Russia walioteuliwa kuongoza maeneo ya Ukraine yaliyochukuliwa kimabavu na Russia hivi karibuni, wamesema kwamba wameanza kuwahamisha maelfu ya watu kutoka miji ya magharibi.

Wamedai kwamba wanajeshi wa Ukraine walipiga feri kwa mabomu na kuua raia wanne.

Wanajeshi wa Russia wamekabiliwa na wakati mgumu yangu mwezi Septemba. Rais Putin ameongeza mashambulizi na hata kutishia kutumia silaha za nyuklia.

Mwezi huu, Russia imeanza kushambulia Ukraine kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, kuharibu mfumo wa umeme na maji wa Ukraine.

Kyiv na mataifa ya magharibi wamesema kwamba uharibifu wa mfumo wa umeme na maji ni sawa na uhalifu wa vita.

Wanajeshi wa Iran wanasaidia Russia

Alhamisi, Marekani imesema kwamba wanajeshi wa Iran wapo Crimea na kwamba wanawasaidia wanajeshi wa Russia kutekeleza mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Ukraine.

"Tunathibitisha kwamba wanajeshi wa Russia walio Crimea wamekuwa wakipewa mafunzo namna ya kutekeleza mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani za Iran, dhidi ya Kyiv,” amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price, katika kikao na waandishi wa habari.

Iran imekanusha madai ya kutoa ndege zake zisizo na rubani kwa Moscow, japo idadi kubwa ya ndege hizi zimeangushwa na Ukraine na kutambuliwa.

"Iran na Russia, zinaweza kudanganya ulimwengu lakini haziwezi kuficha ukweli. Ukweli ni kwamba: Tehran inahusika katika vita hivi moja kwa moja,” amesema msemaji wa maswala ya usalama wa White House John Kirby.

Waziri wa ulinzi wa Ukraine Dmytro Kuleba ameandika ujumbe wa Twitter kwamba amefanya mazungumzo ya kina na waziri mkuu wa Israel Yair Lapid kuhusu ombi la kutaka kupewa mfumo wa ulinzi wa anga na wa kunasa makonbora.

Ofisi ya Lapid imesema kwamba kiongozi huyo wa Israel ameeleza “wasiwasi mkubwa” kuhusu ushirikiano wa kijeshi kati ya Iran na Russia.