Russia inaishutumu Ukraine kwa kutekeleza shambulizi la kinyama

Majengo ya makaazi yaliyoharibiwa katika mji wa Lysychansk

Russia imesema shambulizi hilo liliuwa watu 28 kwenye mji wa Lysychansk wenye wakazi wapatao 110,000 kabla ya uvamizi wa Russia.

Russia leo Jumatatu iliishutumu Ukraine kwa kutekeleza kile Kremlin ilichokiita shambulio la kinyama dhidi ya eneo la kuoka mikate katika mji unaokaliwa na Russia huko mashariki mwa Ukraine.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amelitaja shambulio la Jumamosi huko Lysychansk kuwa ni kitendo cha kigaidi katika miundombinu ya amani. Russia imesema kuwa shambulizi hilo liliuwa watu 28. Mji wa Lysychansk ulikuwa na wakazi wapatao 110,000 kabla ya uvamizi wa Russia. Uliangukia kwa Russia katika majira ya joto ya mwaka 2022, na uko kilomita 15 kutoka eneo linalodhibitiwa na wa-Ukraine.

Maafisa wa Ukraine hawakutoa tamko lolote kuhusu shambulio hilo. Russia na Ukraine zinalaumiana kila mmoja kwa kufanya mashambulizi katika maeneo ya raia, ikiwemo Ukraine inaripoti mara kwa mara makombora ya Russia na mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani ambazo zinalenga miji ya Ukraine.