Russia imeshambulia miji ya Ukraine baada ya kuzuia usafirishaji wa chakula

Ndege ya kijeshi ya Russia ikipaa juu ya makutano ya reli, baada ya kutokea shambulizi la Russia lililosbabisha moto, katika mji wa Shakhtarsk (Shakhtyorsk) karibu na Donetsk, Ukraine, Okt. 27, 2022.

Wanajeshi wa Russia wameushambulia mji mkuu wa Kyiv pamoja na miji mingine kadhaa nchini Ukraine.

Mashambulizi hayo ya makombora yametokea baada ya Moscow kuilaumu Kyiv kwa shambulizi dhidi ya meli zake katika Black Sea, na kujiondoa katika makubaliano ya kusafirisha nafaka kutoka Ukraine.

Russia na Ukraine ni miongoni mwa nchi zinazozalisha kiwango kikubwa cha nafaka duniani.

Hatua ya Russia kuzuia usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine ilisababisha uhaba wa chakula kote duniani mapema mwaka huu.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema kwamba "mashambulizi ya makombora ya Russia yameharibu mifumo muhimu. Badala ya kupigana na wanajeshi, wanawashambulia raia.”

"Huwezi kutetea mashambulizi haya kwa kuyaita kuwa ni majibu. Russia inafanya hivi kwa sababu ina makombora ya kuua raia wa Ukraine.”

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ukraine Oleg Nikolenko, amesema kwamba makombora yameharibu mfumo wa nishati mjini Kyiv na miji mingine, na kusababisha ukosefu wa umeme na maji.

"Russia haionyeshi nia ya kufanya mazungumzo, wala dunia kuwa na chakula. Lengo kubwa la Putin ni kuua na kuharibu.”

Russia haijatoa taarifa yoyote. Imeshutumu Kyiv kwa kushambulia meli zake katika Black Sea katika shambulizi lililotekelezwa na ndege sita zisizokuwa na rubani, Jumamosi.

Mapema mwezi huu, Russia iliushambulia mji wa Kyiv kwa makombora kadhaa, ikisema kwamba ilikuwa hatua ya kujibu shambulizi lililotokea kwenye daraja linalounganisha Russia na Crimea.

Ukraine haijakiri wala kukataa kwamba ilihusika na shambulizi dhidi ya meli za Russia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensiku ameishutumu Russia kwa kutaka kusababisha baa la njaa kote duniani kwa kujiondoa kwenye mkataba wa usafirishaji chakula, uliopatikana baada ya mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa pamoja na Uturuki.

Miongoni mwa meli ambazo zimezuiliwa ni iliyobeba maelfu ya chakula, ilyokodishwa na shirika la chakula la Umoja wa Mataifa, kuelekea Pembe ya Afrika, ambako msaada wa chakula unahitajika kwa dharura.

Ukraine imesema kwamba meli 218 zimezuiliwa. Hakuna meli imeondoka Ukraine tangu Jumapili.