Russia imefanya mashambulizi mapya ya makombora na Drone dhidi ya Ukraine

Mfano wa ndege isiyotumia rubani-Drone aina ya FPV. April 29, 2024. (Photo by Genya SAVILOV / AFP)

Hata hivyo ulinzi wa anga wa Ukraine ulitungua makombora 12 kati ya 16 na Drone zote 13 zilizorushwa na Russia

Russia imefanya mfululizo wa mashambulizi mapya ya makombora na ndege zisizotumia rubani–Drone katika shambulio la usiku kucha dhidi ya Ukraine leo Jumamosi, na kuharibu vituo vya nishati huko kusini mashariki na magharibi, na kuwajeruhi angalau wafanyakazi wawili wa nishati, Maafisa wa Ukraine wamesema.

Ulinzi wa anga wa Ukraine ulitungua makombora 12 kati ya 16, pamoja na Drone zote 13 zilizorushwa na Russia katika shambulio la pili kubwa wiki hii, Jeshi la Anga lilisema. Tahadhari za anga katika mikoa ya Ukraine zilidumu kwa saa kadhaa muda wa usiku.

Mwendeshaji gridi ya taifa Ukrenergo alisema vifaa kwenye vituo vyake katika mkoa wa Zaporizhzhia uliopo kusini mashariki na mkoa wa magharibi wa Lviv iliharibiwa na mashambulizi hayo. Wafanyakazi wawili wa nishati katika mkoa wa Zaporizhzhia wamejeruhiwa na kupelekwa hospitali alisema.