Russia haitaki viongozi wa nchi tajiri kuzungumzia usalama

Rais wa Russia Vladimir Putin Nov. 9, 2022. Putin Hatahudhuria kongamano la viongozi kutoka nchi 20 tajiri zaidi duniani G20, nchini Indonesia.

Russia imeyataka mataifa 20 tajiri zaidi duniani G20, kuacha kujadili kuhusu usalama na badala yake kuangazia zaidi changamoto za kiuchumi zinazoikabili dunia.

Hayo yanajiri wakati viongozi wa G20 wanakutana katika kongamano ambalo limetawaliwa na ukosoaji kutoka kwa mataifa ya Magharibi kuhusu uvamizi wa kijeshi wa Russia nchini Ukraine.

Wizara ya mambo ya nje ya Russia imesema kwamba ni muhimu sana kwa mataifa ya G20 kuangazia zaidi maswala ambayo ni ya uhalisia badala ya kile ilichokitaja vitisho vya kifikra.

Waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergei Lavrov ataongoza ujumbe wa Russia kwenye kongamano hilo ambalo ni la kwanza tangu Russia kuivamia Ukraine mwezi Februari. Kremlin imesema kwamba rais Putin ana kazi nyingi za kufanya na hataweza kuhudhuria kongamano hilo.

Russia imesema kwamba uhaba wa chakula duniani unastahili kuwa ajenda kuu ya mkutano huo wa Bali, unaofanyika siku chache huku muda wa makubaliano wa kusafirisha nafaka katika bahari ya Black Sea, ukielekea kumalizika Novemba 19.