Ross anamatumaini makubaliano ya biashara na China yataafikiwa

Wilbur Ross, waziri wa biashara wa Marekani

Mazungumzo ya ngazi ya waatalamu wa biashara kati ya Marekani na China yalianza Jumatatu huko Beijing wakijaribu kutatua mzozo wa ushuru ambao umetikisa masoko ya dunia katika wiki za karibuni

Waziri wa biashara wa Marekani Wilbur Ross alisema kuna fursa nzuri kwamba Marekani na China watafikia makubaliano ya biashara.

Ross alikiambia kituo cha televisheni cha CNBC kwamba anamatumaini mpango kama huo utashughulikia na kutatua masuala yote muhimu. Mazungumzo ya ngazi ya waatalamu wa biashara kati ya Marekani na China yalianza Jumatatu huko Beijing na wajumbe wa mataifa mawili makubwa kiuchumi wakijaribu kutatua mzozo wa ushuru ambao umetikisa masoko ya dunia katika wiki za karibuni.

Wakati maafisa wa China walielezea matumaini mwanzoni mwa mazungumzo ya siku mbili Beijing wakati huo huo ililalamika kuhusu kuonekana kwa manwari ya Marekani ya USS McCampbell katika kile inachoeleza imeingia ndani ya mipaka ya bahari ya China karibu na visiwa vinavyogombaniwa vya South China Sea.