Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, wamezindua rasimu ya mapendekezo ya kufanyia marekebisho katibu ya nchi hiyo kwa lengo la kusitisha ghasia baada y auchaguzi na masuala mengine ya kisiasa.
Wakati wa sherehe hafla hiyo, naibu wa rais William Ruto ametaka mjadala mpana utakaowashirikisha raia wote wa Kenya kuhusu rasimu hiyo kabla ya kupitishwa.
Rasimu hiyo inapendekeza kubuniwa nafasi ya rais, makam wa rais, waziri mkuu na manaibu wake wawili watakaoteuliwa na rais, Pamoja na kiongozi wa upinzani.
Rais atakuwa na mamlaka ya kumfuta kazi waziri mkuu na manaibu wake.
Mabadiliko hayo yanaunda nafasi ya kiongozi wa upinzani, ambaye atakuwa amemaliza katika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha urais.
Viongozi walihuduria hafla ya uzinduzi wa rasimu hiyo katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi walikuwa na mawazo tofauti kuhusu yaliyomo kwenye rasimu hiyo ya jopo la maridhiano.
Naibu wa rais William Ruto, ambaye hotuba yake ilitatizwa mara kwa mara na baadhi ya wanasiasa waliokuwa katika hafla hiyo, ameonyesha wasiwasi wake kuhusu mapendekezo ya kuundwa kwa baraza la polisi litakaloongozwa na waziri wa usalama, akisema kwamba hatua hiyo itakuwa ya kuingilia uhuru wa polisi.
Ruto vile vile amesema kwamba ripoti hiyo haijajumulisha kila raia wa Kenya serikalini iwapo wote watakaochaguliwa na rais katika serikali wanaweza kutoka chama kilicho madarakani na iwapo kina idadi kubwa ya wabunge.
Ruto vile vile amesema kwamba hatua ya kubadilisha tume ya uchaguzi haifai kwa sasa akisema kwamba vyama vichache vya kisiasa haviwezi kuchagua makamishina wa tume hiyo na waandae uchaguzi huru na haki.
“Ukiniambia ni sawa kwa wengine, na sio timu zote zinazoshiriki, kuteua mwamuzi, nina mashaka yangu kama hiyo ni haki.”Amesema naibu wa rais William Ruto.
Rais Uhuru Kenyatta anaendelea kusisitiza kwamba ripoti hiyo maarufu BBI, itasuluhisha matatizo yanayoikumba Kenya na kwamba ni vizuri kwa raia kuipitisha kupitia kura ya maamuzi.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga, amesema kwamba hatua ya kuifanyia marekebisho katiba ya Kenya ni muhimu katika kukomesha ukabila uliokita mizizi nchini Kenya.
Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi, Kenya.