Rasi wa zamani wa Angola, Dos Santos, amefariki dunia

Rais wa zamani wa Angola, José Eduardo dos Santos, akihudhuria mkutano wa kamati kuu ya chama tawala cha MPLA 2017

Rais wa zamani wa Angola Eduardo dos Santos, aliyetawala kwa karibu miongo minne taifa la pili la Afrika lenye utajiri wa mafuta, amefariki Ijuma, kulingana na afisi ya rais.

Kiongozi huyo wa zamani aliyekua na umri wa miaka 79, alifariki katika zahanati ya Teknon mjini Barcelona, Uhispania ambako alikua anapata matibabu kufuatia ugonjwa wa muda mrefu.

Akiwa miongoni mwa viongozi walotawala kwa muda mrefu barani Afrika, dos Santos aliacha madaraka miaka mitano iliyopita. Utawala wake uligubikwa na vita vye wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu karibu miaka 30 dhidi ya waasi wa kundi la UNITA lililokua linaungwa mkono na Marekani.

Alipata ushindi mwaka 2002, na kushuhudia uzalishaji mkubwa wa mafuta.

Rais Joao Lourenco aliyechukua nafasi yake, ametangaza siku 5 za maombolezi ya kitaifa na kumueleza dos Santos kama "mtu wa kipekee nchini Angola."

Licha ya kwamba alichaguliwa na dos Santos mwenyewe kuchukua nafasi yake, Lourenco mara moja alianza uchunguzi kuhusu tuhuma za ulaji rushwa wa mabilioni ya dola wakati wa enzi ya rais wa zamani.

Rais wa Ureno Marcelo Rebelo de Sousa amesifu uhusiano mzuri ulokiuzwa na dos Santos kati ya nchi zao mbili.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, amesema kiongozi huyo amesaidia katika vita vyao dhidia ya utawala wa wazungu waliokua wachache chini ya mfumo wa ubaguzi wa rangi.