Ramaphosa akabiliwa na uchunguzi wa makosa ya jinai kwa kutoripoti wizi wa dola milioni 4 kwenye shamba lake

Rais Cyril Ramaphosa akijibu masuali ya wabunge mjini Cape Town, March 17, 2022. Picha ya Reuters

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa anakabiliwa na uchunguzi wa makosa ya jinai baada ya taarifa iliyofichuliwa kuwa hakuweza kuripoti wizi wa takriban dola milioni 4 pesa taslimu kwenye shamba lake kaskazini mwa jimbo la Limpopo.

Maelezo kuhusu wizi huo yamo katika hati ya mkuu wa zamani wa ujasusi Arthur Fraser, ambaye alikuwa alianzisha kesi dhidi ya Ramaphosa.

Ramaphosa hakukanusha kwamba wizi huo ulifanyika lakini alidai kwamba aliuripoti kwa mkuu wa kikosi cha ulinzi wake, ambaye hakuripoti wizi huo kwa polisi.

Nchini Afrika Kusini ni kinyume cha sheria kutoripoti uhalifu na kwa mujibu wa hati ya Fraser, Ramaphosa alijaribu kuficha wizi huo, ambao ulitokea Februari mwaka wa 2020 alipokuwa akihudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Vyama kadhaa vya upinzani viliomba kufanyike uchunguzi wa kina kuhusu wizi huo, na kuchunguza ikiwa kiwango hicho cha fedha za kigeni kinachodaiwa kuibwa kiliripotiwa kwenye idara ya mapato ya Afrika Kusini.

Wafuasi wa Ramaphosa wamelalamika wakisema kufichuwa taarifa hiyo wakati huu ni sehemu ya juhudi za kukwamisha juhudi zake za kuwania tena uongozi wa chama chake mwezi Disemba.

Habari kuhusu wizi huo ilifichuliwa na Frazer, mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi, anayejulikana kama mtifu kwa rais wa zamani Jacob Zuma.