Ofisi yake imesema kwamba kiongozi huyo alikuwa hajisikii vizuri na baada ya kufanyiwa vipimo akakutwa kuwa na virusi vya corona. Ripoti zimeongeza kwamba amejiweka karantini mjini Cape Town wakati akiwa chini ya uangalizi wa maafisa wa afya wa kijeshi.
Shughuli zote za serikali zinasemekana kuongozwa na makamu wake David Mabuza kwa sasa. Hata hivyo haijafafanuliwa iwapo Ramaphosa mwenye umri wa miaka 69 anaugua kutokana na virusi aina mpya vya omicron ingawa alikuwa tayari amepokea chanjo kamili hapo awali.
Wiki iliyopita, kiongozi huyo alitembelea mataifa manne ya Afrika magharibi wakati yeye na ujumbe wake wakifanywa vipimo vya covid baada ya kuwasili katika kila taifa. Inasemekana kwamba baadhi ya watu walioandamana naye walipatikana kuwa na virusi nchini Nigeria, na mara moja wakarejeshwa Afrika kusini. Kando na tukio hilo ziara yake inasemekana kuwa salama hadi aliporejea nyumbani Decemba 8 akitokea Senegal.