Katika ujumbe wake wa Twitter, Zelenskyy hakutoa maelezo zaidi kuhusu mazungumzo yake na rais Xi, yakiwa mawasiliano yake ya kwanza rasmi na rais wa China tangu uvamizi wa Russia miezi 14 iliyopita.
Zelenskyy alisema “Ninaamini mazungumzo haya ya simu, vile vile uteuzi wa balozi wa Ukraine nchini China, vitaleta msukumo mkubwa kwa maendeleo ya uhusiano wa nchi zetu mbili.”
Baadaye kwenye tovuti yake, ameyataja mazungumzo hayo kuwa yenye tija na kusema yatatoa mwelekeo wa “uwezekano wa majadiliano kwa lengo la kuweka mazingira ya amani ya haki na ya kudumu nchini Ukraine.”
Vyombo vya habari vya serikali ya China vimeripoti kwamba Xi alitoa wito kwa Zelenskiy kwa ajili ya mazungumzo kati ya Russia na Ukraine, akionya kuwa “hakuna mshindi katika vita vya nyuklia.”