Rais wa zamani wa Mali Amadou Toure afariki

Rais wa zamani wa Mali Amadou Toumani Toure aliyeaga dunia Jumanne tarehe 10 Novemba, 2020.

Rais wa zamani wa Mali Amadou Toumani Toure ambaye alipongezwa sana kwa kufanya mageuzi ya kidemokrasia nchini mwake kabla ya kuondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 2012, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 72.

Maisha ya Toure kwa kiasi kikubwa yalionyesha hali ya kuanza kwa demokrasia nchini Mali, ambapo mrithi wake Ibrahim Boubacar Keita aliondolewa madarakani katika mapinduzi mengine mwezi Agosti.

Toure aliongoza mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 1991 dhidi ya kiongozi wa kijeshi Moussa Traore baada ya maandamano dhidi ya serekali yaliogubikwa na ghasia.

Aliandaa uchaguzi wa kidemokrasia mwaka moja baadaye na kukabidhi madaraka kwa rais raia, na hivyo kupata jina la umaarufu la "Askari wa Demokrasia."

"Toure amefariki dunia Jumatatu usiku nchini Uturuki," afisa muandamizi wa karibu yake Seydou Cissouma ameliambia shirika la habari la Reuters, bila kutoa maelezo zaidi.

Gazeti la Jeune Afrique limeripoti kwamba Toure alisafirishwa nchini Uturuki baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo mjini Bamako.

-Imetayarishwa na Patrick Nduwimana, VOA, Washington DC