Rais wa Tunisia Kais Saied amechaguliwa kwa muhula mwingine kwa asilimia 90.69 ya kura, tume ya uchaguzi ISIE ilisema Jumatatu.
Miaka mitatu baada ya Saied kujinyakulia mamlaka makubwa, makundi ya kutetea haki za binadamu yanahofia kuchaguliwa kwake kutaimarisha utawala wake katika taifa hilo ambalo demokrasia yake iliimarika kufuatia maandamano ya 2011.
Saied, mwenye umri wa miaka 66, alishinda kwa kishindo uchaguzi wa Jumapili kwa kura milioni 2.4, lakini asilimia 28.8 tu ndio walijitokeza kupiga kura kati ya watu milioni 10 wanaotimiza masharti ya kupiga kura.
Mpinzani wake anayefungwa jela Ayachi Zammel alipata asilimia 7.3, na mgombea wa tatu Zouhair Maghzaoui alipata asilimia 1.9 ya kura, kiongozi wa ISIE Farouk Bouasker alitangaza kwenye televisheni ya taifa.