Rais wa Poland anajaribu kumshawishi Tshisekedi amuachie huru raia wa Poland

Rais wa Poland, Andrzej Duda.

Raia huyo wa Poland Mariusz Majewski alikamatwa na vikosi vya Kongo mwezi Februari akishutumiwa kwa ujasusi.

Rais wa Poland Andrzej Duda amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Congo Felix Tshisekedi ili kufanikisha kuachiliwa huru kwa msafiri, raia wa Poland aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela katika nchi hiyo kubwa ya Afrika ya Kati, kwa mashtaka ya ujasusi, msaidizi wake amesema Jumatatu.

Raia huyo wa Poland mwenye miaka 52, Mariusz Majewski, alikamatwa na vikosi vya Kongo mwezi Februari na baadaye alifikishwa katika mahakama ya kijeshi katika taifa hilo, alishutumiwa kwa ujasusi.

Rais Felix Tshisekedi wa DRC.

Tuhuma dhidi yake zilisema kuwa “aliufikia mstari wa mbele kwa wanamgambo wa Mobondo,” alisonga mbele bila idhini na “alipiga picha za maeneo nyeti na ya kimkakati, na kwa siri alichunguza shughuli za kijeshi”.

Mobondo ni kundi la wanamgambo ambalo limekuwa likihusika katika ghasia za kikabila kusini magharibi mwa Congo tangu mwaka 2022.