Rais wa Marekani Joe Biden awasili japan katika mkutano wa G-7

Rasi wa Marekani Joe Biden, kushoto, na waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida, kabla ya mkutano wa G-7 Mei 18.

Biden alipokelewa na kundi la takriban wanajeshi 400 wa Marekani na Japan, katika Kituo cha Marine Corps cha Iwakuni, muda mfupi baada ya kutua.

Kisha alikutana na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida mjini Hiroshima, ambako mazungumzo ya G-7 yanafanyika.

Biden alimwambia Kishida kwamba Marekani na Japan "zinazingatia maadili ya pamoja," ikiwa ni pamoja na kuunga mkono Ukraine na kuiwajibisha Russia kwa vita vyake vya uchokozi. Biden pia alielezea kuhusu azma ya kuhakikisha hali ya kutoenea kwa zana za nyuklia na "kuhakikisha Indo-Pacific huru na wazi."

Mkutano huo wa G-7 pia utajumuisha viongozi kutoka Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Kishida pia alialika kikundi cha wasio wanachama kushiriki katika mkutano huo, kama sehemu ya juhudi za kushirikiana na mataifa ya ukanda wa kusini wa dunia. Mataifa hayo ni pamoja na Australia, Brazil, Comoro, Visiwa vya Cook, India, Indonesia, Korea Kusini, Ukraine na Vietnam.

Viongozi hao wanatarajiwa kujadili vikwazo vya biashara na uwekezaji dhidi ya China, kati ya masuala mengine.