Rais wa Lebanon ameapa hatopumzika hadi wanampata aliyehusika na mlipuko ulioleta maafa

Mlipuko mkubwa umetokea katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, Agosti 4,2020.

Salamu za rambi rambi kwa watu wa Lebanon zimetumwa kutoka sehemu mbali mbali Duniani, ikiwemo jirani zake Israel ambao walisema haraka kwamba hawajahusika na mlipuko huo

Rais wa Lebanon, Michel Aoun anatoa wito kwa baraza la mawaziri kutangaza wiki mbili za hali ya dharura ya kitaifa huko Beirut baada ya mlipuko mkubwa mapema Jumanne ulioharibu sehemu kubwa ya bandari ya mji huo na kuuwa angalau watu 70 na kuwajeruhi zaidi ya 3,500.

Japokuwa chanzo rasmi cha mlipuko huo hakijulikani, Aoun aliandika kwenye mtandao kwamba sitapumzika hadi tunampata mtu aliyehusika na kile kilichotokea na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria na kumhukumu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab alikutana na wizara ya ulinzi Jumanne usiku kwa saa za huko akielezea uungaji mkono wake kwa watu anaowaita “mashahidi” na kuwatakia majeruhi nafuu ya kupona haraka.

Pia alitaka kamati ya uchunguzi iundwe haraka. Diab ametangaza Jumatano ni siku ya maombolezi nchini Lebanon.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema Jumanne wakati akitoa maelezo mafupi kuhusiana na janga la virusi vya Corona huko White House, kwamba "Marekani ipo tayari kuisaidia Lebanon. Tutakuwepo nao kuwapa msaada. Inaonekana ni shambulizi baya sana"