Rais wa Korea Kusini na Waziri Mkuu wa China wakutana

Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk Yeol, na Waziri Mkuu wa China, Li Qiang, Jumapili wamekubaliana kuanzisha mazungumzo ya kidiplomasia na usalama na kuanza tena mazungumzo kuhusu makubaliano ya biashara huru, ofisi ya Yoon imesema.

Yoon na Li walifanya mazungumzo siku moja kabla ya mkutano wao na mwenzao wa Japan, Fumio Kishida, ikiwa ni mazungumzo yao ya kwanza ya njia tatu katika kipindi cha zaidi ya miaka minne.

Yoon alimwambia Li nchi hizo mbili zinapaswa kufanyakazi pamoja sio tu kukuza maslahi yao kwa kuheshimiana, lakini pia katika masuala ya kikanda na kimataifa ili kukabiliana na changamoto za pamoja, akitoa mfano vita vya Ukraine, mzozo wa Israel na Hamas na uchumi wa dunia kutokuwa wa uhakika.