Rais wa Iraq Fouad Massoum Jumatatu alimteua mwanasiasa mkongwe wa dhehebu la Shia Haidar Abadi kuunda serikali mpya baada ya mvutano mrefu na waziri mkuu anayeondoka Nouri al-Maliki, ambaye amekataa kuondoka madarakani. Mara tu baada ya uteuzi huo bwana Maliki alionekana kwenye televisheni akiwa na wanasiasa wa kundi lake akisisitiza kuwa hatakubali uteuzi huo na kwamba yeye (Maliki) atabaki kama Waziri Mkuu.
Televisheni ya Asharqiya iliripoti kuwa walinzi wa rais pia walikuwa katika hali ya juu ya tahadhari kulinda makao yake alipokuwa anateuwa Waziri Mkuu mpya.
Katika hotuba yake kupitia televisheni Bw. Maliki alimshtumu rais Fouad Massoum kwa kukiuka katiba kwa kuchelewesha uteuzi wa Waziri Mkuu mpya. Alitoa mwito kwa mahakama ya juu ya Iraq kumshinikiza Bw. Massoum kuteuwa kundi analoongoza la kisiasa kuunda serikali mpya, kwa sababu lina viti vingi bungeni. Hata hivyo bw. Abadi anatoka katika muungano wa kisiasa wa bw. Maliki.
Wakati huo huo rais wa Marekani Barack Obama amewasihi wale wanaofanya kazi ya kuunda serikali mpya waungane pamoja kwa lengo la kuondoa kitisho cha wanamgambo wa kiislam Islamic State, ambao wamedhibiti sehemu kubwa ya nchi hiyo.