Rais wa Russia Vladimir Putin Jumapili amewasili katika mji mkuu wa Uzbekistan ambako atafanya mazungumzo na Rais Shavkay Mirziyoyev, ambayo yanatarajiwa kulenga kuimarisha uhusiano wa nchi hizo.
Putin aliweka shada la maua katika mnara wa uhuru wa Uzbekistan huko Tashkent na kushikilia kile Kremlin ilisema kuwa mazungumzo yasiyo rasmi na Mirziyoyev. Mkutano rasmi wa viongozi hao unatarajiwa kufanyika Jumatatu.
Ziara hiyo ni ya tatu kwa Putin tangu alipoapishwa kwa muhula wa tano mwezi Mei. Kwanza alikwenda China, ambako alielezea kufurahishwa na mapendekezo ya China katika mazungumzo ya kumaliza mzozo nchini Ukraine, na baadaye Belarus ambako Russia imepeleka silaha za nyuklia.
Kabla ya ziara ya Uzbekistan, Putin na Mirziyoyev walijadili masuala kadhaa ya ushirikiano wa nchi hizo mbili, ikijumuisha mahusiano ya biashara na kiuchumi, Kremlin ilisema.