Rais Samia ashuhudia utiaji saini makubaliano ya awali ya mkataba wa mradi wa LNG

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akishuhudia utiaji saini Mkataba wa Awali wa Mradi wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia (Liquefied Natural Gas – LNG Project) kwenye Hafla iliyofanyika tarehe 11 Juni 2022 Ikulu, Chamwino Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini ya makubaliano ya awali ya mkataba wa mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia na kampuni za Equinor ya Norway na Shell ya Uingereza.

Hafla ya utiaji saini huo imefanyika Jumamosi katika Ikulu ya Chamwino Dodoma.

Rais Samia amesema mradi huo ni wa kimkakati kwa nchi ambao utakapokamilika utauingizia nchi mapato na kuinua uchumi. Mradi huu pia utazalisha ajira na kuchangia katika kujenga uwezo wa watanzania kupitia mafunzo, elimu, kuinua teknolojia na utafiti.

Hivyo, Rais Samia ametoa wito kwa vijana kujiandaa ili kuwa na ujuzi na weledi wa kutosha kuweza kuchangamkia fursa zitakazojitokeza.

Aidha, Rais Samia ameelekeza majadiliano yatakayoendelea juu ya Mkataba huo yasimamie maslahi ya nchi na kuhakikisha mikoa ya Lindi na Mtwara inapata manufaa zaidi katika mradi huo.

Rais Samia pia amesema dhamira ya Serikali ni kuona vizazi vijavyo vinavuna rasilimali za nchi kwa tija, manufaa, na kujitegemea zaidi.

Vile vile, Rais Samia ameziagiza taasisi za udhibiti, kodi, na usimamizi wa sheria kujiimarisha ili nchi iweze kwenda na mahitaji mahsusi ya uwekezaji na biashara hii.

Maamuzi ya mwisho ya uwekezaji (FID) yanatarajiwa kufikiwa mwaka 2025 na baada ya maamuzi hayo ujenzi wa mradi huo utachukua miaka mitano kukamilishwa.