Rais Ruto aapa kukabiliana na waandamanaji wanaopinga mswaada wa fedha

Rais wa Kenya akifanya mahojiano na shirika la habari la AFP huko Seoul wakati wa mkutano wa Korea na Afrika Juni 5, 2024. Picha ya AFP

Rais wa Kenya, William Ruto, katika hotuba kwa taifa Jumanne, amesema kuwa matukio ya vurugu yaliyoshuhudiwa Jumanne ambapo waaandamanaji walivunja ua wa bunge na kuingia ndani na kusababisha uharibifu mkubwa, ni kitendo cha uhaini.

“Cha kusikitisha zaidi ni kwamba mashambulizi ya leo (Jumanne) dhidi ya utaratibu wa kikatiba wa Kenya yamesababisha watu kupoteza maisha, uharibifu wa mali na kuzibeza taasisi na nembo za mamlaka yetu,” Ruto anasema.

Ruto ameongeza kuwa serikali yake itatimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuwalinda raia wa Kenya dhidi ya kila aina ya madhara, na kuwaonya wale alioataja ni “wapangaji, wafadhili, waandaaji na watetezi wa ghasia na machafuko” yaliyoshudiwa Jumanne jijini Nairobi na miji mingine ya nchi hiyo.

“Si jambo la haki na kistaarabu kufikiriwa kwamba wahalifu wanaojifanya waandamanaji wa amani wanaweza kusababisha ugaidi na vurugu dhidi ya wananchi, wawakilishi wao waliowachagua na taasisi zilizoanzishwa chini ya katiba yetu na kutarajia kuachiliwa huru,” rais Ruto amekariri.

Ruto anadai kuwa maandamano hayo yalitekwa nyara na wahalifu hatari ambao wamelisababishia taifa hasara na hivyo ameviagiza “vyombo vyote vya usalama vya taifa kuchukua hatua zote za kuzuia majaribio yoyote ya wahalifu hatari ya kuhujumu usalama na utulivu wa nchi yetu.”

“Nalihakikishia taifa, kwamba Serikali imekusanya rasilimali zote kwa ajili ya taifa ili kuhakikisha kwamba hali ya aina hii, haitajirudia tena, kwa gharama yoyote ile.”

Hata hivyo, Ruto hajaeleza iwapo ataridhia malalamiko ya wananchi kwa kufanyia marekebisho ya mswaada wa fedha uliozua utata.

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, ametangaza kuwa anasimama na raia wa Kenya na kuitaka serikali ya rais Ruto kuwasikiliza wananchi badala ya kutumia nguvu zinazoweza kuliweka taifa kwenye njia panda na vurugu zaidi.

"Ninakuja kwenu nikiwa na huzuni kubwa ya kupoteza maisha kutokana na hali ya sasa nchini. Ni haki ya Wakenya kuandamana kama ilivyoamuliwa na Katiba ya Kenya ya 2010. Pia ni wajibu wa viongozi kuwasikiliza wanaowaongoza," Kenyatta amesema.

Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta

"Kama rais wenu wa zamani nimehisi uzito wa kuwaongoza Wakenya. Kwa hivyo naomba hekima na ustaarabu uimarishwe na amani na maendeleo yawe yetu sote kama watoto wa Kenya," ameongeza.

Wakenya wanaofanya maandamano makubwa katika miji mikuu wanaendelea kuongeza shinikizo kwa serikali ya Rais Ruto kuuondoa kabisa Mswaada wa Fedha wa 2024 uliobeba makato ya ushuru kufadhili bajeti ya 2024/25 na ambayo yameibua joto jingi.

Bunge la taifa Jumanne, limepitisha mswaada huo, wabunge 195 walipiga kura ya NDIO huku wabunge 100 wakipiga kura ya LA, na rais Ruto anatarajiwa kuufanya kuwa sheria wakati wowote.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Mwandishi wetu wa Nairobi, Kenya.