Nchi hiyo ya Afrika ambayo imeendelea kiviwanda iliongoza kampeni ya kutaka chanjo zitengenezwe katika bara la Afrika, na kuwa mtengenezaji wa kwanza na mkubwa wa chanjo ya Covid 19.
“Mashirika ya kimataifa ambayo yalipewa pesa nyingi za kununua chanjo kwa ajili ya nchi maskini hayanunui chanjo zilizotengenezwa Afrika, hata zile chanjo ambazo zinatumwa kwa nchi za Afrika,” Ramaphosa ameuambia mkutano wa kimataifa kuhusu Covid kwa njia ya mtandao.
“Hali hii lazima ibadilike,” Ramaphosa amesema katika hotuba yake kwa mkutano huo wa pili wa kimataifa kuhusu Covid ambao uliongozwa na Rais wa Marekani Joe Biden.
Kampuni kubwa ya Afrika Kusini ya kutengeneza dawa Aspen, wiki iliyopita ilitoa taarifa ya kusisimua kwamba haijapata zabuni yoyote ya chanjo ya Covid iliyotengenezwa Afrika kwa ajili ya Afrika, ambayo iliidhinishwa na kampuni ya Marekani Johnson and Johnson, na kutishia kufunga kiwanda chake cha uzalishaji isipokuwa tu ikipata zabuni.