Rais Putin aapa kwamba Russia itaendelea kuishambulia Ukraine.

Rais Vladimir Putin akitoa hotuba yake katika kiwanda cha kuunganisha makombora ya roketi nje ya mji wa Tsiolkovsky, April 12, 2022. Picha ya AP.

Rais wa Russia Vladimir Putin Jumanne ameapa kwamba nchi yake itaendelea na mashambulizi dhidi ya Ukraine hadi Moscow itakapokamilisha malengo yake na kudai kwamba vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na nchi za magharibi vitakuwa na athari kwa Marekani na washirika wake.

Katika matamshi yake ya kwanza hadharani kuhusu vita hivyo katika kipindi cha zaidi ya wiki moja, Putin amesema kwamba Shambulio la Moscow dhidi ya nchi jirani ya Ukraine linaendelea kulingana na mpangalio, ingawa Russia imekiri kupoteza idadi kubwa ya wanajeshi.

Matamshi ya Putin yanajiri wakati Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson walizungumza kuhusu ziara ya Johnson ya wiki iliyopita nchini Uktraine.

White House imesema viongozi hao wawili wamethibitisha dhamira yao ya kuendelea kutoa msaada wa kiusalama na kibinadamu kwa Ukraine katika kukabiliana na vitendo vya kikatili vinavyoendelea kufanywa na Russia na wamepongeza ushirikiano unaoendelea na washirika wao kwa kuiwekea vikwazo Russia kwa kuendesha vita bila kuchokozwa na bila sababu inayoeleweka.