OBAMA: Mshambuliaji wa Orlando hana uhusiano wa moja kwa moja na magaidi

Rais wa Marekani, Barack Obama, amesema Jumatatu kuwa hakuna ushahidi kuwa mtu aliefanya mauwaji ya halaiki kwenye klabu cha watu mashoga mjini Orlando, Florida alikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kundi la kigaidi kutoka nje ya nchi.

Akihutubia wanahabari kwenye Ikulu ya Marekani, ameongeza kusema inaonekana kwamba mshambuliaji huyo alipata mafunzo kupitia mtandao wa Internet.

Obama amesema kuwa Omar Saddiqui Mateen, mwenye umri wa miaka 29, ni muislamu aliezaliwa Marekani na wazazi wenye asili ya Afghanistan na ameonyesha ugaidi wa ndani ya nchi ambao Serikali yake imekuwa ikihofia kwa muda mrefu.

Seddique Mateen, baba ya mshambuliaji wa Orlando

Ikulu imesema kuwa Rais atasafiri kuelekea Orlando leo Jumanne ili kutoa pole kwa familia za walioathiriwa.

Kiongozi wa shirika la kijasusi la 'FBI,' James Comey, amesema kuwa wanaendelea kuchunguza maisha ya mshambuliaji na hasa matumizi yake ya mtandao wa internet.