Rais Ndayishimiye anapanga kuwaachia wafungwa na kuboresha magereza

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye

Wafungwa wanaotumikia hadi  kifungo cha miaka mitano wanastahili msamaha wa rais, isipokuwa wale wanaochukuliwa kuwa hatari kwa usalama wa taifa

Burundi inapanga kuwaachia maelfu ya wafungwa ili kupunguza msongamano magerezani katika taifa hilo la Afrika mashariki. Wafungwa wapatao 5,255 au takribani asilimia 40 ya idadi ya wafungwa wataachiwa huru, kulingana na amri iliyoonekana kupitia shirika la Habari la Ufaransa-AFP.

Rais Evariste Ndayishimiye ameripotiwa akisema msamaha huo ulikuwa hatua muhimu kupunguza msongamano na kuboresha hali kwenye magereza. AFP inasema wafungwa wanaotumikia hadi kifungo cha miaka mitano wanastahili msamaha wa rais, isipokuwa wale wanaochukuliwa kuwa hatari kwa usalama wa taifa.

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya ufisadi wataachiliwa kwa masharti ya kulipa fedha walizotumia vibaya, ikiwemo uharibifu na gharama za mahakama. Kuachiliwa huru kwa wafungwa kunakuja zaidi ya miezi miwili baada ya Rais Ndayishimiye, kutia Saini amri ya kuwaachia huru waandishi wa Habari wanne katika hatua iliyotangazwa sana baada ya kutoa ahadi za kupunguza mbinu kali zilziotumiwa na mtangulizi wake.