Rais wa Uganda atangaza baraza la Mawaziri

Yoweri Museveni

Mke wake atangazwa waziri wa elimu na michezo

Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni ametangaza baraza lake la mawaziri Jumatatu mjini Kampala na kumtaja mke wake bibi Janet Museveni kuwa waziri wa elimu na michezo.

Rais Museveni ambaye amekuwa madarakani kama Rais wa Uganda kwa zaidi ya miaka 30, alitangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa urais uliofanyika mwezi wa pili mwaka huu kwa zaidi ya asilimia 60.

Bi Janet Museveni atashikilia wadhifa nyeti wa uwaziri wa elimu na michezo, nafasi ambayo inatajwa ni muhimu sana nchini Uganda kwa sababu ya kutumia bajeti kubwa sana ya serikali.

Andrew Karamagi, mwanasheria wa haki za binadamu ameliambia shirika la habari la kimataifa la Reuters kuwa baraza la mawaziri limelenga zaidi kuweka uwiano kwenye dini na ukabila ili kupata msaada zaidi wa kisiasa na sio kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.

Msemaji wa serikali, Shaban Bantariza amekanusha madai hayo akisema Museveni yuko makini sana na watu aliowachagua.