Rais Museveni aamuru wanajeshi zaidi kwenda magharibi mwa Uganda kuwasaka ADF

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Jumapili ametoa amri ya kupelekwa wanajeshi zaidi upande wa magharibi wa Uganda ambako washambuliaji kutoka kundi lenye uhusiano na Islamic State limeuwa takriban wanafunzi 37 wa shule ya sekondari.

Wanamgmbo wa kundi la uasi na kigaidi la Allied Democratic Forces (ADF) waliwaua wanafunzi hao Ijumaa jioni katika shule ya sekondari ya Lhubirira iliyoko wilaya ya Mpondwe, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wanajeshi na polisi wamesema washambuliaji hao pia walikuwa wamewateka nyara wanafunzi sita na kutorokea katika hifadhi ya taifa ya Virunga baada ya kuvuka mpaka.

Hatima yao mpaka sasa haijulikani kulingana na taarifa.

Rais Museveni amesema wanajeshi zaidi walijiunga na msako huo katika eneo hilo, ambalo ni pamoja na Mlima Rwenzori, ambapo ADF ilianzisha uasi wake dhidi ya serekali ya Museveni katika miaka ya 1990.