Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa siku ya Alhamisi alisema enzi ya uingiliaji kati wa Ufaransa barani Afrika imekwisha alipoanza ziara ya mataifa manne ya bara hilo ili kurejesha uhusiano uliotetereka.
Hisia za chuki dhidi ya Ufaransa zimeongezeka katika baadhi ya makoloni ya zamani ya Afrika wakati bara hilo likizidi kuwa uwanja wa vita vya kidiplomasia, huku ushawishi wa Russia na China ukiongezeka katika eneo hilo.
Macron alisema Ufaransa haina nia ya kurejea sera za zamani za kuingilia bara la Afrika.
Enzi ya Francafrique imepita, Macron alisema katika hotuba yake kwa jamii ya Wafaransa katika mji mkuu Libreville, akimaanisha mkakati wa Ufaransa wa baada ya ukoloni wa kuunga mkono viongozi wa kimabavu kutetea maslahi yake.