Rais Joe Biden wa Marekani, ametangaza mpango mpya wa msaada wa kijeshi kwa Ukraine, Alhamisi, katika mkutano wa NATO, hapa Washington.
Biden ametoa tangazo hilo kuhusu msaada wa dola milioni 225 wakati wa mkutano na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy.
Msaada wenye thamani hiyo kutoka kwa mamlaka ya ‘Drawdown’ ya Rais utajumuisha uwezo wa kusaidia Ukraine kurudisha nyuma vikosi vya Russia. Miongoni mwa vitu vilivyojumuishwa ni betri za makombora ya Patriot, mifumo ya taifa ya makombora ya ardhini mpaka angani (NASAMS), makombora ya kushambulia ndege, na risasi za mifumo ya roketi za juu za HIMARS.
Rais Zelenskyy amemshukuru Rais Baiden na kuongeza kuwa Ukraine pia inahitaji baadhi ya hatua za haraka kuondoa vikwazo kwa askari wa Ukraine, akimaanisha vikwazo ambavyo Marekani inaweka kwenye matumizi ya silaha zake.