Rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kujadili mvutano katika Mashariki ya Kati na timu yake ya usalama wa taifa leo Jumatatu, na kufanya mazungumzo ya simu na Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan, huku viongozi wa Israel wakionya watajibu kwa “gharama kubwa” kama watashambuliwa, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa na Iran au washirika wake katika eneo hilo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amesema katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu kwamba Iran haitafuti kuongeza mvutano katika eneo hilo, lakini ina haki ya kuiadhibu Israel kufuatia shambulio la wiki iliyopita lililomuua kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh mjini Tehran.
Iran inailaumu Israel kwa mauaji ya Haniyeh, ambayo yamekuja saa chache baada ya shambulizi la anga la Israel mjini Beirut lililomuua kamanda wa kundi la wanamgambo la Hezbollah, ambalo ni kundi kama vile Hamas linaloungwa mkono na Iran.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Jumapili kwamba Iran na washirika wake wanataka kuizingira Israel katika “mkakati wa ugaidi”.