NASA yawasilisha kesi mahakama ya juu Kenya

Raila Odinga akizungumza baada ya kukabidhiwa hati na IEBC. Raila na muungano wa NSA waliwasilisha kesi kwenye mahakama ya juu mnamo tarehe 18 mwezi Agosti, 2017.

Muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA, Ijumaa usiku uliwasilisha malalamiko kwenye mahakama ya juu, kupinga uchaguzi wa rais Uhuru Kenyatta uliotangazwa wiki moja iliyopita na tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC.

Mawakili wa muungano huo waliwasilisha nyaraka zao katika mahakama ya juu mjini Nairobi saa tatu na nusu za usiku.

Hatua hiyo ilikuwa imesubiriwa na wafuasi wengi wa muungano huo, baada ya aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya NASA, Raila Odinga, kutangaza siku ya Jumatano kwamba wangewasilisha hoja yao mahakamani.

Raila na wenzake kwenye muungano huo wanashikilia kwamba uchaguzi wa mwaka huu uligubikwa na dosari na kwamba yeye ndiye aliyestahiki kutangazwa mshindi.

Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, mahakama ya juu inazo siku 14 za kusikiliza na kuamua kesi hiyo.

Kufuatia uchaguzi uliofanyika siku ya Jumanne tarehe 8 mwezi Agosti, IEBC ilitangaza kwamba Kenyatta alishinda kwa kura 8,203,290 huku Raila Odinga akipata 6,762,224.

Odinga amesema kuwa ushindi huo wa Uhuru si halali na kwamba ulikarabatiwa na kompyuta.

Jaji mkuu wa Kenya David Maraga, amesema kwamba mahakama ya juu iko tayari kufanya kazi usiku na hata wikendi ili kusikiliza na kuamua kesi hiyo katika muda uliowekwa kikatiba.

Kuapishwa kwa rais ambako kulikuwa kumepangwa sasa kumeahirishwa hadi pale mahakama itakapotoa uamuzi wake.