Kesi ya washukiwa sita wa ghasia za mauaji ya uchaguzi mkuu uliopita inaendelea kuchukua sura na msimamo mpya nchini kenya. Zikiwa zimesalia wiki mbili tu kabla ya washukiwa wa ghasia hizo kufika mbele ya mahakama ya kimataifa ya icc mjini Hague mgawanyiko mkubwa unaendelea kujitokeza katika serikali ya muungano na pia kwenye chama cha ODM.
Waziri mkuu Raila Odinga anasema ikiwa chama chake cha ODM kitaidhinisha kufunguliwa kwa mashtaka hayo nchini Kenya basi itabidi majasusi na makachero wa kimataifa wa Scotland Yard ya Uingereza na shirika la upelelezi la marekani - FBI kutekeleza uchunguzi wa kesi hizo kwasababu polisi wa nchini humo ni baadhi ya washukiwa,
Akizungumza kwa hasira katika majengo ya bunge mjini Nairobi, waziri mkuu Odinga amesema hana imani na upelelezi wa polisi wa Kenya kwasababu wao ni baadhi ya watuhumiwa wa ghasia hizo, na kuongezea kuwa ni lazima kuwepo na majasusi walio huru na wenye uwezo wa kusimamia uchunguzi huo.
Matamashi ya waziri mkuu yamezusha shutuma na lawama kali kutoka kwa waziri wa sheria na katiba Bwana Mutula Kilonzo, akipinga vikali pendekezo la kuwahusisha majasusi wa kimataifa kama vile Scotland Yard na FBI katika uchunguzi huo, anasema uchunguzi uliofanywa awali na mashirika hayo mawili haukufua dafu.
"Je katiba hii tumepitisha ya kufanya nini kama tungali tutakuwa tunauliza Scotland Yard na FBI waje kama tulivyofanya wakati wa shambulizi la bomu kwenye ubalozi wa marekani na pia wakati wa kifo cha Robert Ouko," anasema waziri Kilonzo.
Suala hili la mahakama ya ICC limekuwa ni nyeti kwa serikali na hasa chama cha Raila Odinga cha ODM.
Washukiwa watatu wanaotuhumiwa kwenye mahakama ya ICC ni wanachama wa ODM, na baadhi ya wafuasi wa Raila Odinga wanadai itakuwa ni busara kugharamia matumizi yote ya wanachama wa ODM wanaotuhumiwa katika mahakama ya ICC.
Serikali ya Kenya inaendelea kukabiliwa na mgawanyiko mkubwa kutokana na kesi inayowakabili washukiwa sita wa ghasia za uchaguzi mkuu.