Raila amesema kuwa udukuzi huo umepelekea kile alichokiita majumuisho ya kura yalioghushiwa yakionyesha kwamba yeye yuko nyuma kabisa katika kinyang’anyiro hiki ya Rais Uhuru Kenyatta.
Tovuti ya IEBC imeonyesha mchana Jumatano kuwa asilimia 94 ya kura zilizopigwa tayari zimehisabiwa na zinaonyesha Kenyatta anaongoza kwa asilimia 54 wakati yeye ana asilimia 45 katika kinyang’anyiro cha awamu ya pili.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amesema hawezi kusema lolote kuhusu mfumo wa tume hiyo kuwa umedukuliwa, lakini itafanya uchunguzi.
Odinga aliwasomea waraka waandishi ukieleza tuhuma zake kwamba wadukuzi waliingia katika mfumo wa takwimu za IEBC wakati wa kupiga kura Jumanne na kubadilisha matokeo sio tu kwa uchaguzi wa urais lakini katika chaguzi za nafasi nyingine.
Lakini Rafael Tuju, katibu mkuu wa chama cha Jubilee, alitupilia mbali tuhuma za Odinga kwamba sio kweli na kutaka kuwepo utulivu.
“Matokeo haya hayaji bila ya utaratibu, yanathibishwa na ukweli, na huwezi kufanya madai kwamba matokeo ni feki kuhusiana na uchaguzi wa urais na kukubali matokeo ya maeneo ambayo magavana wako wameshinda na wabunge wako pia wameshinda.
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amesema Jumatano kuwa wadukuzi wamefanya wizi mkubwa kwenye mfumo ya kompyuta ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.