Wazambia wanapiga kura hii leo katika uchaguzi wenye mvutano mkali ambapo rais na mpinzani wake mkuu wamesema ni mtihani kwa hadhi ya taifa hilo la kusini mwa Afrika kama demokrasia thabiti.
Upigaji kura ulianza mapema leo asubuhi katika uchaguzi wa urais na wabunge katika vituo zaidi ya 12,000, pamoja na kwenye magereza. Zaidi ya watu milioni 7, au zaidi ya asilimia 83 ya wapiga kura wanaostahiki, wamejiandikisha kupiga kura, kulingana na Tume ya Uchaguzi ya Zambia.
Rais Edgar Lungu anategemea kushinda kura kutokana na rekodi yake ya maendeleo ya miundombinu, hasa inayofadhiliwa na China, na usambazaji wa pembejeo za kilimo kama mbegu na mbolea kwa mamilioni ya wakulima.
Hata hivyo, nafasi yake inaweza kuwa hatarini kutokana na mabadiliko ya mabaya ya kiuchumi. Lungu, ambaye aliingia madarakani mwaka 2015, alipiga kura yake katika mji mkuu, Lusaka.