Raia mmoja wa Israel amepatikana ameuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa Palestina kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi Jumamosi asubuhi, jeshi la Israel limesema wakati ghasia zikiongezeka katika eneo hilo linalokaliwa kimabavu.
Jeshi limesema mtu huyo alitangazwa kuwa amekufa baada ya kupigwa risasi katika mji wa Qalqilya, na kwamba vikosi vya Israel kwa sasa vinafanya kazi katika eneo hilo. Tangazo hilo la Jumamosi limekuja siku moja baada ya vikosi vya Israel kuwaua kwa kuwapiga risasi wanamgambo wawili katika mji huo wa Ukingo wa Magharibi. Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kwa umma.
Ghasia zimezuka Ukingo wa Magharibi tangu vita vya Israel na Hamas vilipozuka mwezi Oktoba mwaka jana. Tangu wakati huo, Wapalestina wasiopungua 549 katika eneo hilo wameuawa kwa kupigwa risasi na Israeli inasema Wizara ya Afya ya Palestina, ambayo inafuatilia mauaji hayo.
Wakati huo huo, Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wamewaua takriban Waisraeli tisa, wakiwemo wanajeshi watano, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.