Putin atembelea Mariupol

Kremlin inasema kwamba rais wa Russia, Vladimir Putin aliutembelea mji wa bandari wa Mariupol wa  Ukraine unaoshikiliwa na Russia.

Ziara hii imefanyika baada ya kuitembelea peninsula ya Crimea kuadhimisha mwaka wa tisa toka Moscow kuingia kimabavu kinyume cha sheria mwaka 2014.

Kiongozi huyo wa Russia aliwasili Mariupol, Jumamosi jioni, kwa mujibu wa msemaji wa Kremlin, Dmitryn Peskov, ambapo picha za video zimemuonyesha rais Putin akizungumza na wakazi wa mji huo baada ya ziara ya mapema katika shule ya Sanaa na kituo cha watoto huko Crimea.

Ziara hiyo imefanyika baada ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu – ICC – Ijumaa kutoa hati ya kukamatwa kwa rais Putin, kwa uhalifu wa kivita wa kukamata watoto wa Ukraine katika uvamizi huo wake wa miezi 13 nchini Ukraine.