Ureno imeishangaza dunia na kuingilia himaya ya timu kubwa za kandanda Ulaya kwa kushinda kombe la Euro 2016 kwa mara ya kwanza katika historia kwa kuwafunga wenyeji Ufaransa 1-0 katika dakika za nyongeza.
Ureno walifanikiwa kupata ushindi huo bila mchezaji wao nyota na nahodha wa timu hiyo ya taifa Cristiano Ronaldo ambaye alilazimika kuondoka uwanjani baada ya kuumia goti katika dakika 25 tu za mwanzo wa mchezo
Wareno walijikusanya vizuri baada ya nahodha wao kuondoka uwanjani na kusaidia na mlinda mlango Rui Patricio ambaye aliokoa magoli mengi langoni kwake. Eder ndio alikuwa nyota wa mechi kwa upande wa Ureno kuipatia timu yake bao la ushindi la zikiwa zimebakia dakika 11 kabla muda wa nyongeza kumalizika.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ureno kuifunga Ufaransa ambayo imeshinda mechi zote 10 zilizopita baina yao.
Ureno ilionekana kufika fainali ya Euro 2016 kwa kusua sua huku timu kubwa kama Ujerumani, Spain na Uingereza zikitolewa katika hatua za mwanzo hadi semi fainali. Wachambuzi wengi wa kandanda walidhani Ufaransa ina nafasi nzuri ya kushinda fainali hasa kwa vile inachezea nyumbani lakini hadi kipenga cha mwisho alikuwa nahodha wa Ureno Ronaldo aliyekuwa akibusu kombe la Euro 2016.