Pompeo : Tathmini ya kiintelijensia yaihusisha Iran na mlipuko wa meli

Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo

Jeshi la majini la Marekani, limetoa video inayoonyesha boti ya Iran inayofanya doria katika Ghuba ya Oman ikiondoa bomu lililokuwa halijaripuka liliokuwa pembeni ya meli ambalo halijalipuka kutoka katika moja ya meli ya mafuta iliyoshambuliwa Alhamisi.

“Tathmini hii inatokana na taarifa za kiintelijensia, silaha zilizotumika, kiwango cha weledi ulihitajika kutekeleza operesheni hiyo, mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na Iran katika meli nyengine na ukweli kwamba hakuna kikundi kinachopingana katika eneo hilo ambacho kina rasilmali na weledi wa kutekeleza shambulizi hilo kwa kiwango cha ujuzi huo uliotumika katika shambulizi hilo," amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.

Ameongeza kuwa : "Hili ni tukio pekee la hivi karibuni katika mashambulizi kadhaa yaliyo shawishiwa na Jamhuri ya Kiislam ya Iran na vikundi vyake vinavyo fanya hujuma dhidi ya maslahi ya Marekani na washirika wake."

Waziri Mike Pompeo, anailaumu Iran kwa shambulizi lililotokea Alhamisi, dhidi ya meli mbili za mafuta katika Ghuba ya Oman, nje kidogo na pwani ya Iran, ikiwemo moja iliyoteketezwa kwa moto.

Mojawapo ya meli hizo inamilikiwa na Norway na nyingine inamilikiwa na kampuni ya Japan.

Taarifa zaidi zinasema bomu hilo lilikuwa limepachikwa katika meli ya Japan, pembeni ya bomu ambalo tayari lilikuwa limeripuka. Meli ya Norway iliripuliwa na kuwaka moto.