Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo anatarajiwa kukutana Jumatano jioni huko New York na Jenerali wa ngazi ya juu Korea Kaskazini.
Wanakutana kwa ajili ya kuandaa maongezi kabla ya mkutano uliopangwa kati ya Rais Donald Trump na kiongozi wa Korea kaskazini.
Pompeo atakutana na Kim Yong Chol, makamu mwenyekiti wa Kamati Kuu ambayo ina madaraka makubwa na mkuu wa zamani wa ujasusi wa Korea Kaskazini. Wamekutana tayari mara mbili huko Pyongyang.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa Pompeo atakuwa New York mpaka Alhamisi, kwa hivyo huenda watu hao wawili wakawa na mikutano zaidi.