Polisi Tanzania wasema Watanzania wanahusika katika mashambulizi mpakani na Msumbiji

kambi ya wakimbizi, Cabo Delgado

Jeshi la polisi Tanzania limesema kwamba raia wa Tanzania wanahusika na mashambulizi yanayofanyika mpakani mwa Msumbiji na Tanzania.

Kamishna wa oparesheni na mafunzo katika jeshi la polisi Tanzania Liberatus Sabas, amesema kwamba baadhi ya mashambulizi yanayotokea katika eneo la kusini mwa Tanzania mpakani na Msumbiji yanafanywa na vijana waliotoroka Tanzania baada ya kufanya vitendo kama hivyo katika mikoa ya pwani na Tanga.

Liberatus Sabas amesema kwamba licha ya matukio hayo ya mashambulizi kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa jamii ya watanzania inatakiwa kufuatialia kwa karibu sana mienendo ya vijana katika jamii ili kukomesha hali ya vijana kujiunga na makundi ya uhalifu.

Amesema kwamba baadhi ya vijana hao walitoroka shule na kujiunga na makundi hayo.

Polisi Tanzania wamesema kwamba watu kadhaa wamekamatwa wakihusishwa na matukio hayo ya mashambulizi kati ya Tanzania na Msumbiji.

Ukamataji huo unaendelea kwa ushirikiano wa maafisa wa usalama wa Tanzania na Msumbiji.

Nyumba kadhaa ziliteketezwa moto, watu kuuawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya Cabo Delgado, Msumbiji.