Polisi wa DRC walijitokeza kwa nguvu Jumatatu kusitisha maandamano ya upinzani yaliyopigwa marufuku mjini Kinshasa kudai kutoegemea upande wowote kwa tume ya uchaguzi na kuwakamata watu kadhaa mwandishi wa shirika la habari la AFP aliripoti. Kufikia mapema asubuhi hii leo kwa saa za huko vikosi vya usalama vilikuwa vimefunga barabara zote za kuingia katika makao makuu ya tume ya uchaguzi mjini humo.
Ofisi za tume huru ya kitaifa ya uchaguzi (CENI) zipo kati kati mwa jiji la Kinshasa. Takribani waandamanaji 100 walijitokeza na mara moja wakasambaratishwa na polisi ambao pia waliwakamata baadhi ya waandamanaji.
Angalia uwepo huu wa polisi, ilikuwa kama tuko vitani, alieleza kwa kukasirika mmoja wa waandamanaji, Fidele Likinda, mbunge wa chama cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD).
Mkuu wa polisi, Sylvano Kasongo, aliwaambia waandishi kuwa kikosi cha polisi kitaendelea kuwepo mtaani kwa siku nzima kama ikibidi. Idadi kadhaa ya vyama na vuguvugu la makundi ya kanisa vilitoa wito wa maandamano kupinga uteuzi wa hivi karibuni wa mshirika wa Rais Felix Tshisekedi kuongoza CENI.