Polisi Kenya wavamia shule ya Kiislamu na kuwakamata walimu 2

Maafisa wa polisi nchini Kenya

Maafisa wa polisi nchini Kenya

Polisi wa Kenya walivamia shule moja ya kiislamu Jumanne na kuwakamata waalimu wawili, kuwachukua takriban watoto 100 na kuwaweka chini ya ulinzi kwa kile ambacho polisi imekielezea kuwa ni operesheni ya kukabiliana na ugaidi na kuhusisha idara za polisi za kigeni.

Polisi walisema shule hiyo iliyo katika eneo la Likoni, kusini mwa mji wa bandari wa Mombasa, kama kituo cha kuwafunza vijana wa kiume na watoto itikadi na uanamgambo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, chanzo cha polisi ambacho kimehojiwa kwa misingi ya kutotajwa jina kimesema, “sehemu hiyo ilikuwa ikifuatiliwa kwa muda mrefu.” Msemaji wa polisi Kenya hakupatikana kutoa maoni yake.

Kiongozi mmoja wa kiislamu katika eneo hilo alithibitisha kuwepo kwa operesheni hiyo lakini amesema hakuna ushahidi wa harakati zozote ambazo ni kinyume cha sheria.

“Kundi la maafisa wa polisi wa ndani na wa kigeni lilivamia madrasa ambako wanafunzi walikuwa wamelala wakati huo na kuwachukua waalimu wao,” Sheikh Hassan Omar, afisa mwandamizi wa baraza la Maimamu na Wahubiri Kenya (CIPK), taasisi mwamvuli ya viongozi wa dini Kenya, aliwaambia wanahabari mjini Mombasa.

“kuna tarkiban wanafunzi 100 na waalimu wanne wa madrasa ambao wamekamatwa na kuzuiliwa kwenye makao makuu ya polisi na hakuna anayetueleza ni uhalifu gani waliotenda,” alisema Omar.

Bado haiko bayana kwanini polisi na CIPK walitoa maelezo tofauti kuhusu idadi ya waalimu waliokamatwa.