Polisi nchini Kenya wamewataka waandamanaji kuepuka kuandamana hadi uwanja wa ndege wa mji mkuu na viunga vyake, huku taasisi ya kuendesha uwanja huo ikiwataka abiria kufika saa kadhaa kabla ya safari za ndege kutokana na kuimarishwa kwa ukaguzi wa usalama.
Maandamano yanayoongozwa na vijana kote nchini Kenya kupinga mapendekezo ya nyongeza ya kodi yameendelea hata baada ya Rais William Ruto kuondoa sheria hiyo mwishoni mwa mwezi Juni na kuwafuta kazi takriban mawaziri wote.
Alitangaza sehemu ya baraza lake jipya la mawaziri siku ya Ijumaa, huku akiwabakiza baadhi kutoka kwenye baraza la mawaziri alilolifuta.
Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamejipanga kuandamana hadi kwenye uwanja wa ndege, jambo lililosababisha polisi kutoa onyo.
Wanaharakati wanasema wanataka Ruto ajiuzulu na wanataka kufanyike mageuzi ili kusafisha ufisadi na kushughulikia utawala duni na utoaji huduma katika serikali za kitaifa na kikanda.