Polisi haiwahusu nani atanipokea uwanja wa ndege - Bobi Wine

Bobi Wine

Muda mfupi baada ya polisi kutoa muongozo wa hatua za usalama zinazo chukuliwa wakati Mbunge wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine ataporejea kutoka Marekani, msanii nyota huyo ameapa kukaidi amri hizo.

"Nimekuwa najiuliza kwa nini hawa maafisa wa polisi wanakubali kujidhalilisha kiasi hicho.Wanataka kuamua nani aje kunipokea na wapi nielekee baada ya kuwasili? Basi, kwa taarifa yenu, hakuna hata mwana familia mmoja ambaye atanipokea uwanja wa ndege, nitakutana nao nyumbani kwa sababu najua namna ya kufika nyumbani! Nitapokelewa na marafiki, viongozi wenzangu na wasanii wengine. Baada ya hapo nitakwenda na kumuona bibi yangu ambaye ni mgonjwa kwa muda mchache kitongoji cha Najjanankumbi na baada ya hapo nitaelekea Kamwokya kupata chakula cha mchana na wanafamilia (kaka na dada zangu) kabla ya kuelekea nyumbani kijijini Magere,” amesema Bobi Wine katika tamko alilotuma katika mitandao yake ya jamii Jumatano mchana.

Vyanzo vya habari nchini Uganda vimeripoti kuwa mapema Jumatano, msemaji wa Polisi, Emilian Kayima amewaambia waandishi wa habari mjini Kampala kuwa atakapowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Entebbe Alhamisi, mbunge huyo atapokelewa na familia yake na atapatiwa ulinzi kutoka uwanja wa ndege mpaka nyumbani.

“Polisi itaendelea kuhakikisha watu wanaotumia barabara wako salama. Hakutaruhusiwa mikutano, maandamano na mikusanyiko ilikuwa kinyume cha sheria. Harakati zozote ambazo zitahusisha mikusanyiko lazima zifuate sheria,” amesema Kamanda Kayima.

Lakini, Kyagulanyi amejibu kwa kusema: “ Mimi ni mwananchi wa Uganda huru ambaye nina uhuru wa kuzunguka nchini kwangu.

Polisi sio jukumu lao kunipangia mimi nani anipokee na nani hawezi kunipokea au wapi naruhusiwa kwenda na wapi siruhusiwi. Vizuizi hivi lazima vikome mara moja. Nitakutana nanyi marafiki zangu kesho,”