PLO Lumumba asema EACC haitamaliza ufisadi Kenya

Lumumba asema lazima viongozi wawajibike kutokana na rushwa Kenya

Na Kennedy Wandera

NAIROBI: Kufuatia kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa tume ya kupambana na ufisadi nchini Kenya, Philip Kinisu, aliyekuwa mkurugenzi wa tume hiyo kwa wakati mmoja, Dkt PLO Lumumba, alielezea hisia zake kuhusu hatua hiyo, na kusema kuwa kubadilisha maafisa wa tume hiyo hakusaidii kwa vyovyote katika juhudi za kupambana na ufisadi nchini humo.

Akizungumza na Sauti ya Amerika siku ya Jumatano, Lumumba, ambaye aliondolewa kutoka kwa uongozi wa tume hiyo kwa tuhuma za kutowajibika, alisema kwamba mkondo ambao vita dhidi ya ufisadi unachukua ni wa kuvunja moyo.

"Ni lini tutaona wanasiasa ambao wamehusishwa na ulaji rushwa wakishtakiwa na kufungwa," aliuliza Lumumba.

"Hata akiwekwa mwenyekiti mwinggine, ataondolewa tu," aliongeza.

Kinisu alijiuzulu siku ya Jumatano baada ya kamati ya bunge kuhusu sheria na haki kupendekeza kwamba rais Uhuru Kenyatta aundejopo la kumchunguza Kinisu ambaye amekuwa kwenye afisi hiyo kwa takriban miezi minane.

Alimwandikia rais Kenyatta barua ya kujiuzulu, na kusema kuwa anaamini fedha na wakati unaotumiwa kumchunguza, ungetumika kwa kushughulikia maswala mengine muhimu.

Kabla ya tume hiyo kutoa kauli hiyo, baadhi ya Wakenya walimtaka Kinisu ang’atuke afisini mara moja. Lakini afisa huyo amekuwa akishikilia kwamba hakuwa na hatia yoyote kumlazimu kuondoka.

Kinisu anahusishwa na kampuni ya Esaki, ambayo inatuhumiwa katika sakata ya National Youth service (NYS) inayoaminika kuifuja serikali mamia ya mamilioni ya pesa. Esaki nadaiwa kupewa kandarasi ya kutoa huduma katika shirika la NYS.

Madai yaliyomkabili ni kwamba kampuni hiyo ililipwa shilingi milioni 35.4 kwa huduma ya kuchimba visima, kati ya shughuli nyengine.

Lakini Kinisu ameshikilia kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na mkewe, na kwamba hakujua lolote kuhusu shughuli zake tangu alipojiuzulu. Hata hivyo tetesi zimeibuka kwamba alijiuzulu baada ya tarehe aliyopeana kwa wachunguzi.

Haya hapa mahojiano kati ya PLO Lumumba na Sauti ya Amerika:

Your browser doesn’t support HTML5

PLO LUMUMBA