Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius anaitembelea Ukraine leo Jumanne katika kuonyesha kuiunga mkono nchi hiyo kwenye vita vyake dhidi ya uvamizi wa Russia ulioanza takribani miaka mitatu iliyopita.
Maafisa wa Ujerumani wamesema ziara hiyo inalenga kuihakikishia Ukraine kuwa itaendelea kupata msaada, huku Pistorius anakutana na maafisa wa ngazi ya juu wa Ukraine. Ziara hiyo inakuja chini ya wiki moja kabla ya kuapishwa kwa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump na maswali kuhusu namna sera ya Marekani kuelekea Ukraine inaweza kubadilika chini ya utawala mpya.
Maafisa katika mikoa kadhaa ya Russia wamesema Jumanne kuwa maeneo yao yalishambuliwa na ndege zisizo na rubani za Ukraine, ikijumuisha Saratov ambako Gavana Roman Busargin alisema kulikuwa na uharibifu katika makampuni mawili ya viwanda katika miji jirani ya Saratov na Engels.
Eneo hilo ni kituo cha ndege za kivita za Russia. Wiki iliyopita shambulio la Ukraine liligonga ghala la mafuta ambalo linahudumia kituo hicho.