Pervez Musharraf azikwa katika makaburi ya kijeshi Karachi

Maafisa wa jeshi na raia wakihudhuria mazishi ya Rais wa zamani wa Pakistan Pervez Musharraf huko Malir Garrison huko Karachi, Pakistan Februari 7, 2023.

Sala ya mwisho ilifanyika Jumanne mjini Karachi kwa ajili ya Pervez Musharraf, hayati  rais wa zamani wa  Pakistan na mtawala wa kijeshi.

Ibada hiyo katika uwanja wa kambi ya kijeshi ilifanyika saa chache baada ya mwili wa Musharraf kusafirishwa kwa ndege maalum hadi mji wa bandari wa kusini kutoka Dubai, ambako yeye na familia yake walikaa miaka yake ya mwisho katika uhamisho wake . Miongoni mwa waliohudhuria ni wakuu wa zamani wa kijeshi Qamar Javed Bajwa, Ashfaq Parvez Kayani na Aslam Beg.

Waziri Mkuu wa sasa Shehbaz Sharif hakuhudhuria, lakini alitoa ujumbe wa rambirambi kwenye Twitter akisema "natoa rambirambi zangu kwa familia ya Jenerali Pervez Musharraf. Roho ya marehemu ipumzike kwa amani!

Musharraf alizikwa katika makaburi ya kijeshi huko Karachi.

Musharraf alifariki Jumapili huko Dubai akiwa na umri wa miaka 79 kutokana na amyloidosis, ugonjwa adimu ambapo protini isiyo ya kawaida hujilimbikiza kwenye viungo, na kusababisha kutofanya kazi vizuri. Aliingia madarakani Oktoba 1999 baada ya kumpindua Waziri Mkuu aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia Nawaz Sharif, kaka wa waziri mkuu wa sasa, katika mapinduzi yasiyo na umwagaji damu.