Papa Francis ayataka makanisa Sudan Kusini kupaza sauti dhidi ya udhalimu

Baba Mtakatifu Francisko akisalimiana na waumini Wakatoliki kutoka mji wa Rumbek, waliotembea kwa zaidi ya wiki moja kufika mji mkuu, baada ya mkutano katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Teresa, Juba, Sudan Kusini, tarehe 4 Februari 2023.

Papa Francis alisema Jumamosi Makanisa nchini Sudan Kusini hayawezi kutoelemea upande wowote  lazima yapaze sauti zao dhidi ya udhalimu na matumizi mabaya ya madaraka, huku yeye na viongozi wengine wawili wa Kikristo wakiendesha harakati za  amani katika nchi hiyo mpya zaidi duniani

Katika siku yake ya kwanza kamili nchini Sudan Kusini, Francis aliwahutubia maaskofu, mapadre na watawa wa Kikatoliki katika kanisa kuu la Mtakatifu Theresa katika mji mkuu Juba wakati Askofu Mkuu wa Canterbury na mkuu wa Kanisa la Scotland walifanya ibada sehemu nyingine.

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 lakini ikatumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 huku makabila yakishambuliana. Licha ya makubaliano ya amani ya mwaka 2018 kati ya wapinzani wakuu wawili, mapigano ya kikabila yameendelea kuua na kuwakosesha makazi raia wengi.

"Ndugu na dada, sisi pia tunaitwa kuwaombea watu wetu, kupaza sauti zetu dhidi ya dhuluma na matumizi mabaya ya madaraka ambayo yanakandamiza na kutumia vurugu ili kukidhi malengo yao," Francis alisema na kuongeza kuwa viongozi wa kidini "hawawezi kubaki upande wowote mbele ya maumivu yanayosababishwa na vitendo vya udhalimu".

Kuna wakimbizi wa ndani milioni 2.2 nchini Sudan Kusini, kati ya jumla ya wakazi wapatao milioni 11.6, na wengine milioni 2.3 wameikimbia nchi hiyo kama wakimbizi, kulingana na Umoja wa Mataifa.