Papa Francis awapandisha vyeo makasisi 21 kuwa makadinali

Papa Francis akimbariki Kadinali mpya Mons.Claudio Gugerotti, wakati wa hafla ya kuwapandisha vyeo makasisi wa Kanisa Katoliki kuwa makadinali, kwenye uwanja wa Mtakatifu Petro, Septemba 30, 2023.

Papa Francis Jumamosi aliwapandisha vyeo makasisi 21 kutoka maeneo ya mbali duniani, kuwa makadinali, akisema kuwa kujumuisha watu kutoka maeneo tofauti ni hatua muhimu kwa mstakabali wa Kanisa Katoliki.

Huku jua likiwa limewaka, na umati wa watu ukijaza nusu ya mji wa Vatican kwenye uwanja wa mtakatifu Petro, Papa Francis mwenye umri wa miaka 86 aliwakaribisha makadinali hao wapya wanaoitwa “Wana mfalme wa Kanisa” ambao mmoja wao siku moja anaweza kuwa mrithi wa papa wa sasa.

“Baraza la makadinali linatakiwa kufanana na bendi ya muziki, ambayo inawakilisha uelewano na msingi wa kanisa, amesema Francis.

Kuchagua makadinali wapya, wakiwemo wanadiplomasia, washauri wa karibu na wasimamizi, kunaangaliwa kama kiashiria cha vipaumbele na nafasi ya Kanisa Katoliki.

Mmoja kati yao anaweza kuchaguliwa na wenzake siku moja kumrithi Francis, ambaye alisema yuko tayari kujiuzulu katika siku zijazo iwapo sababu za kiafya zitamlazimu kufanya hivyo.