Papa Francis atolewa hospitali

Papa Francis ameruhusiwa kutoka hospitali ya Roma, Jumamosi alikokuwa akitibiwa na kuwatania waandishi wa habari alipokuwa anaondoka kuwa bado "yupo hai."

Papa Francis, 86, alilazwa katika hospitali ya Gemelli Polyclinic siku ya Jumatano kufuatia mkutano wake na waumini kila wiki katika uwanja wa St. Peter baada ya kuripotiwa kupata matatizo ya kupumua.

Katika ishara ya kuimarika kwa afya yake, Vatican ilitoa maelezo ya ratiba ya wki takatifu ya Papa Francis.

Ilisema kuwa ataongoza misa ya Jumapili ya Matawi wikiendi hii na misa ya Pasaka hapo Aprili 9, zote zitafanyika katika uwanja wa St Peter na inatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya waumini.

Kardinali wa Vatican atakuwa madhabahuni kuadhimisha misa zote mbili, kutokana na papa kuwa na tatizo la goti.

Lakini Papa Francis amepangwa kuendesha misa ya Alhamisi Kuu, ambayo mwaka huu itafanyika katika gereza la watoto huko Roma.

Bado haijulikani kama atahudhuria tukio la usiku la Msalaba katika Ukumbi wa Colosseum wa Roma kuadhimisha Ijumaa Kuu.

Kabla ya kuondoka Gemelli Polyclinic Jumamosi asubuhi, Papa Francis aliwafariji wanandoa wa Roma ambao binti yao mwenye umri wa miaka 5 alikufa Ijumaa usiku katika hospitali ya Kikatoliki.